MAANA YA NAMBA 10 KIBIBLIA NA UHUSIANO WAKE NA FUNGU LA KUMI (ZAKA) | LUKAZA BLOG

MAANA YA NAMBA 10 KIBIBLIA NA UHUSIANO WAKE NA FUNGU LA KUMI (ZAKA)

Moja ya swali ambalo watu wengi wamekuwa wakiuliza ni juu ya zaka au fungu la kumi. Ni matumaini yangu kuwa post hii itakusaidia kuelewa ...

Moja ya swali ambalo watu wengi wamekuwa wakiuliza ni juu ya zaka au fungu la kumi. Ni matumaini yangu kuwa post hii itakusaidia kuelewa maana ya namba 10 kibiblia na kwa nini zaka ni 10%.
10 ni namba ya “ukombozi” au “redemption.” Ukisoma Kutoka 12 utaona kuwa siku ya 10 ndiyo siku ambayo wana wa Israel waliambiwa kutwaa “mwana—kondoo” ili waile pasaka na kunyunyiza damu katika vizingiti vya mlango ili Mungu atapoenda kuwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, wazaliwa wao wa wana wa Israel wasiuawe.
Siku hii ya kumi ndio siku ndio ilikuwa siku ya mikate isiotiwa chachu. Ukisoma habari za Yesu pia ni hivyo hivyo. “Hata siku ya kwanza, ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, ni wapi utakapo tukuandalie uile pasaka” (Matayo 28:17).
Kwa hiyo siku ya 10 ndiyo ilikuwa siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu – Pasaka. Na sisi tunajua katika damu ya Yesu ndio kuna ukombozi. Kwa hiyo ilikuwa siku hii ambapo Yesu alitoa damu yake kwa ajili ya ukombozi.
Katika ulimwengu wa roho, siku hii ndiyo ilikuwa siku Yesu alitoa damu yake. Msalabani Yesu alienda kulikamilisha hili kwa jinsi ya mwili lakini damu ya agano ilitolewa katika siku hii ya mikate isiyotiwa chachu kama ilivyokuwa katika Kutoka 12 (siku ya 10 ya mwezi ule).
“Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndio damu ya agano, imwagikayo kwa ajili yenu na wengi kwa ondoleo la dhambi” (Matayo 26:27—28).
Kwa hiyo namba 10 inasimama badala ya ukombozi. Ndio maana sisi nasi tunatakiwa tumpatie Mungu 10% ya KILA KITU.
Moja ya vitu ambavyo 10% inafanya ni kutukomboa na laana iliyoachiliwa kwenye ardhi mwanadamu alipoasi. Maandiko yanatuambia ardhi ililaaniwa Adamu alipoasi” (Mwanzo 3:17).
Ila hatuoni kwenye Biblia mahali panaposema ile laana iliondolewa. Tunapompa Mungu 10% yake, moja ya vitu vinaachiliwa ni ondoleo la laana ya ardhi ambayo Mungu aliiweka dhambi ilipoingia.
Fungu la kumi linaachilia ni uhalali wa madirisha ya mbinguni kufunguliwa katika maisha ya mtu (Malaki 3:10).
Hapa ndipo tunapopata sababu ya kwa nini 10% inatakiwa kwenda kwa Mungu. Kwenye fungu la kumi hapa ndipo kuna aina ya mahubiri au mafundisho huyapati kwenye dini. Biblia haisemia 10% ya mshahara peleka mahali unaposali ila dini ndio inasema hivyo.
Maandiko yanatuambia fungu la kumi linapelekwa “kwa Mungu.” Sasa swali la kujiuliza ni “Kwa Mungu” ni wapi? Kwa watu wengine “kwa Mungu” maana yake “kanisani.” Shida ni kwamba tunachoita leo “kanisa” na kile biblia inasema ni tofauti.
Kwa sababu hiyo, watu wengi inapofika kwenye zaka, wanatoa kidini na siyo kibiblia, kwa kuwa wamefundishwa/wamehubiriwa kidini zaidi kuliko kibiblia. Wote tunajua kabisa hakuna “jengo la kanisa” lolote lile duniani lililojengwa kwa mikono ya wanadamu ambapo Mungu yumo.
Maandiko yanatumbia “miili yetu ndiyo hekalu la Mungu” (1 Wakorintho 6:19). Kwa sisi ni hekalu la Roho Mtakatifu, kitu cha kwanza na cha muhimu zaidi cha kumpa Mungu ni miili yetu.
Mimi nataka tuliangalie suala la zaka kiupana na siyo tu kitendo cha kupeleka 10% ya mshahara kanisani. Ndio maana sehemu nyingi watu wanapojadili juu ya fungu la kumi, mjadala mkubwa upo kwenye jinsi ya kutoa pesa huku wakiulizana: je ninatoa kabla ya makato au baada ya makato? Je wapi kwenye biblia inasema fungu la kumi ni kutoa pesa?? Zaka ni zaidi ya kutoa pesa.
Maandiko yanatuambia “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake” (Zaburi 24:1). Kwa hiyo hiyo 100% ni kila kitu ni cha Mungu. Pamoja na kwamba 10% unampelekea lakini hata 90% unayobaki nayo ni ya Mungu.
Shida kubwa ya leo ni kwamba watu wengi wamelelewa kidini zaidi kuliko kibiblia. Fungu la kumi siyo tu 10% ya mshahara bali ni 10% ya KILA KITU.
Tuangalie mfano kwa Yakobo: “Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika KILA UTAKALONIPA, hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi” (Mwanzo 28:22).
Yakobo hakusema atatoa 10% ya pesa bali ya kila kitu. Sasa je: Ni mangapi Mungu amekupa?? Shida ni kwamba dini imewapa watu fikra ya kwamba fungu la kumi linalotakiwa ni pesa au vitu mtu anavyopata kwa jinsi ya mwili.
Kwa sababu hiyo kwa watu wengi kutoa fungu la kumi ni kutoa sehemu ya kumi ya mshahara wao. Lakini ukisoma maandiko inatakiwa fungu la kumi la KILA KITU.
Tuangalie mfano huu halisi: Maandiko yanatuambia 10% ya KILA KITU; muda nao upo ndani ya hivi vitu. Kwa hiyo katika masaa 24, masaa mawili na dakika 40 kila siku lazima umpatie Mungu.
Hivyo mtu ambaye hatoi angalau masaa 2 na dakika 40 kila siku kwa Mungu, anamuibia Mungu sawa na yule ambaye hatoi sehemu ya kumi ya mapato yake kwani mwizi ni mwizi haijalishi anaiba nini.
Ila kwa nini hatufundishwi hivi katika makanisa yetu? Kwa sababu katika dini nyingi pesa ni muhimu zaidi kuliko muda. Ndio maana huwezi kusikia sana dini ikifundisha kumpa Mungu asilimia kumi ya muda wako kila siku ila watakuhimiza tu kupeleka 10% ya mapato yako kanisani.
Halafu kuhakikisha kwamba fungu la kumi hupeleki kwingine, wanakuambia fungu la kumi lazima upeleke kanisani unaposali.
Ila Mungu mwenyewe ndiye anatakiwa akupe maelekezo ya kufanya juu ya fungu la kumi lake. Kumbuka fungu la kumi ni la Mungu. Kwa hiyo Mungu ndiye anayeamua namna gani litumike. Ila kwa watu kwa watu wengi dini zao ndio ndio zinaamua jinsi ya kulitumia fungu la kumi la Mungu.
Kwa sababu hiyo, inapofika kwenye suala la zaka, katika ulimwengu wa roho, watu wengi wameunganishwa zaidi na dini zao kuliko Mungu aliyetoa agizo la kutoa zaka.
Sisi wote tunajua ya kuwa muda ni mali zaidi ya pesa. Kwa hiyo mtu anayempa Mungu 10% ya muda wake kila siku anatoa zaidi ya yule anayetoa 10% tu ya kila pesa anayopata kwani muda una thamani zaidi kuliko pesa. Ndio maana hakuna kitu kibaya kama kupoteza uaminifu kwa Mungu katika muda kwani kila kusudi lina muda wake (Mhubiri 3:1).
Hivyo mtu ambaye hampi Mungu angalau masaa mawili na dakika arobaini ya kila siku maandiko yanatuambia ni mwizi. Sasa niulize kila mmoja hapa: ni nani amekuwa mwizi wa muda kwa Mungu? Naamini kila mmoja wetu hapa kwa namna moja au nyingine atanyosha mkono.
Kwa hiyo inapofika kwenye fungu la kumi, maandiko yanatuambia ni 10% ya KILA KITU ila dini ndiyo inasisitiza kwenye 10% ya pesa kwani kila dini inachotaka zaidi ni pesa. Mafarisayo walikuwa watu wa dini na maandiko yanatuambia walikuwa watu ambao wanapenda pesa (Luka 16:14).
Natumaini hii imekupa kitu fulani juu ya maana ya namba 10. Ukitaka kuingia ndani kidogo utaona kuwa fungu la kumi siyo tu 10% bali asilimia 10% ya kwanza. Pia Mungu ndiye anayekupa maelekezo zaka itumikaje na wakati mwingine Mungu ataenda tofauti na mchungaji wako.
Kila mzaliwa wa kwanza ni wa Mungu. Katika Agano la Kale watu walikuwa wanachukua sehemu ya kumi, kwa mfano, ya wanyama wao halafu utasikia wakichoma moto kama sadaka ya kuteketezwa. Ndio maana hata Yeriko, mji wa kwanza kabisa kutekwa na wana wa Israel chini ya Joshua, Mungu alitoa maelekezo wauchome moto.
Natumaini umepata kitu cha kukusaidia juu ya namba kumi ambalo litakufanya uone kuwa fungu la kumi ni zaidi ya pesa ambayo umekuwa unatoa. Mungu anataka kwanza maisha yako na muda wako kwani hivyo ni muhimu zaidi ya pesa.
Maandiko yanatuambia “Sadaka ya wasio haki ni chukizo” (Methali 21:27). Hivyo Mungu anataka kwanza moyo wako na muda wako naye kabla ya sadaka yako ya pesa.
Maombi yangu kwako Mungu akupe kujua thamani yako kwake ili ujitoe kwake na kuutafuta ufalme wake kwanza (Matayo 6:33).
Kuutafuta ufalme wa Mungu kwanza ni pa moja na kumpa Mungu muda wake. Natumaini sasa utaanza kutoa zaka ya muda kila siku katika kusoma maandiko, kuomba, na kumsikia Mungu anasema nini nawe.
Ubarikiwe sana,
Jacob & Devotha Makaya
Kingdom of Heaven Ministry

Related

Hot Stories 9095544446008193183

Post a Comment Default Comments

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)

emo-but-icon

SEDUCE ME BY ALI KIBA

TMT 2016.FILAMU NDIO SISI

Winner ABA 2015

BOOK ME - YOUR JOB NEEDS ME

All Recent Posts

>

Connect Us

item